Prof Ikingura Aongoza Kikao cha 20 Bodi ya GST
Asisitiza juhudi na ubunifu kazini
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Prof. Justinian Ikingura ameongoza Kikao cha 20 cha Bodi ya Taasisi hiyo ambapo ameitaka Menejimenti ya GST kuongeza juhudi na ubunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali.
Hayo ameyasema leo Oktoba 24, 2024 katika kikao cha Bodi ya GST kilichofanyika kwenye ukumbi wa Prof. Abdulkarim Mruma uliyopo Jijini Dodoma ambapo wajumbe wa Bodi hiyo na Menejimenti ya GST wameshiriki.
Aidha, Prof. Ikingura amesisitiza kuhakikisha ukusanyaji wa sampuli za miamba za kuhifadhiwa katika Makumbusho ya Jiolojia (Geological Museum) unafanyika wakati wa ugani na kuweka mwongozo wa namna bora ya ukusanyaji wa sampuli hizo.
Katika hatua nyingine, Prof. Ikingura ameielekeza Menejimenti ya GST kuhakikisha inatangaza kwa Umma matokeo na umuhimu wa tafiti zinazofanywa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuufahamisha Umma.
Pamoja na mambo mengine, Prof. Ikingura ameipongeza GST kwa kuendelea kumiliki Ithibati ya Ubora katika utoaji huduma za Maabara iliyoipata Mwaka 2015 baada ya kukidhi viwango vya Kimataifa vya utoaji wa huduma za Maabara.
Pia, Prof. Ikingura imeielekeza Menejimenti ya GST kuendelea kufuatilia upatikanaji wa Ithibati ya Vyungu vya kuyeyushia sampuli za madini ya dhahabu ili kuwaridhisha na kuwahakikishia watumiaji wa bidhaa hiyo.
Vikao vya Bodi ya GST hufanyika mara nne kwa Mwaka ambapo ni kila baada ya kila robo ya kila Mwaka wa Fedha ambapo Kikao cha 20 cha Bodi hiyo kimelenga kujadili taarifa ya Utekelezaji wa GST kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2024.