Taarifa Kuhusu Matetemeko ya Ardhi yaliotokea Mkoani Dodoma

Wakala unapenda kuufahamisha umma kwamba kulikuwa na matukio ya matetemeko ya ardhi ambayo vitovu vyake vilikuwa katika maeneo ya Haneti Mkoani Dodoma umbali wa kati ya kilomita 72 hadi 79 kaskazini Mashariki ya mji wa Dodoma. Matetemeko hayo yenye ukubwa wa kati ya 1.5 na 4.7 katika kipimo cha Richter yaliweza kusababisha mitikisiko ambayo ilisikika katika maeneo mengi ya mkoa wa Dodoma. Taarifa hizi kama ambavyo zimeoneshwa katika jedwali hapo chini zimenakiliwa kutoka katika kituo cha kuratibu matetemeko ya ardhi kilichopo Dodoma mjini:-

Tarehe Muda wa tukio Latitudo (KUS) Longitudo (MAS) Ukubwa Kina
4/12/2017 08:24:10.83 Mchana 5 33.24¹ 36 3.8¹ 2.6 Richter Km 15
4/12/2017 03:53:0.39 Usiku 5 36.30¹ 36 2.2¹ 1.5 Richter Km 15
5/12/2017 08:57:0.15 Usiku 5 40.85¹ 36 14.5¹ 4.7 Richter Km 15
5/12/2017 11:40:26.91 Alfajiri 50 37.97¹ 36 9.0¹ 3.5 Richter Km 15

Mpaka sasa wakala haujapata taarifa za kutokea kwa madhara kutokanana na matetemeko hayo ingawa baadhi ya wananchi wa maeneo ya Haneti na Dodoma mjini wamethibitisha kwamba mitikisiko ilikuwa mikubwa kiasi cha kusababisha hofu hususan tukio lililotokea majira ya saa 8 usiku.
Wakala unaendelea kufanya mawasiliano katika maeneo mbalimbali ili kupata taarifa kuhusiana na matukio hayo. Aidha wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari kama ambavyo wamekuwa wakielekezwa na wataalamu wa mitetemo ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na matetemeko ya ardhi. Wananchi pia wanashauriwa kutoa taarifa kwa uongozi wa maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa mitetemeo ya ardhi katika maeneo husika kwa wakati.

Kwa mawasiliano zaidi na ushauri wasiliana nasi kwa namba 0262323020 au 0754310570

Imetolewa na
Kitengo cha Majanga ya Asili
5/12/2017