Taarifa kuhusu tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 25 mei 2017 mkoani geita

Mnamo tarehe 25 Mei 2017 majira ya saa 06:55:28.29 mchana kulitokea tetemeko la ardhi ambalo lilisikika katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita. Tetemeko hilo pia lilisikika katika miji ya Mwanza, Shinyanga na Ushirombo. Tetemeko hilo lilizua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa mkoa wa Geita na Shinyanga na kusababisha taharuki kubwa. Wakala unaendelea kufanya mawasiliano ili kupata taarifa zaidi kutoka maeneo mbalimbali.

Aidha Wakala ulichakata takwimu za mitetemo ya ardhi zilizonakiliwa kutoka katika kituo chake cha Dodoma ambazo zilionesha kwamba kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kaskazini mashariki ya mji wa Geita ambapo ni magharibi ya mji wa Sengerema likiwa na ukubwa unaofikia kiasi cha 5 katika kipimo cha Richter. Hata hivyo takwimu hizo ni za awali ambazo huenda zikawa na mabadiliko kidogo pindi Wakala utakapo kusanya takwimu kutoka kwenye vituo vingine na kuzichakata.

Wakala unawashauri wananchi katika maeneo hayo kuendelea kuchukua hatua za tahadhari kwani huenda mitetemo ikaendelea kujirudia.
Imetolewa na:
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
25 Mei 2017