TAARIFA KUHUSU TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA TAREHE
25 MEI 2017 MKOANI GEITA

Mnamo tarehe 25 Mei 2017 majira ya saa 06:55:28.29 mchana kulitokea tetemeko la ardhi ambalo lilisikika katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Geita. Tetemeko hilo pia lilisikika katika miji ya Mwanza, Shinyanga na Ushirombo. Tetemeko hilo lilizua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa mkoa wa Geita na Shinyanga na kusababisha taharuki kubwa. Wakala unaendelea kufanya mawasiliano ili kupata taarifa zaidi kutoka maeneo mbalimbali.

Aidha Wakala ulichakata takwimu za mitetemo ya ardhi zilizonakiliwa kutoka katika kituo chake cha Dodoma ambazo zilionesha kwamba kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kaskazini mashariki ya mji wa Geita ambapo ni magharibi ya mji wa Sengerema likiwa na ukubwa unaofikia kiasi cha 5 katika kipimo cha Richter. Hata hivyo takwimu hizo ni za awali ambazo huenda zikawa na mabadiliko kidogo pindi Wakala utakapo kusanya takwimu kutoka kwenye vituo vingine na kuzichakata.

Wakala unawashauri wananchi katika maeneo hayo kuendelea kuchukua hatua za tahadhari kwani huenda mitetemo ikaendelea kujirudia.

Imetolewa na:
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
25 Mei 2017


TAARIFA KWA UMMA YA TUKIO LA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA

1    Tukio la tetemeko:

Tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kumetokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba (Picha Namba 1 na 2). Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi kwenye eneo hilo.


 
Picha Namba 1:     Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Mduara)

 
Picha Namba 2:     Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Nyota nyekundu)

Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa. Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikijumuisha nyumba nyingi kupasuka (Picha Namba 3 na 4), watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyuma ambapo inakisiwa kuwa watu 13 wamepoteza maisha yao.
 

Picha namba 3:    Nyumba iliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.